Hekima ya Mungu

Sulemani na Akina Mama Wawili

Video hii imepakuliwa kutoka Vimeo. Chini ya video, bofya "Download", kisha uchague ubora wa video unaotaka.


Marejeo ya Maandiko: 1 Wafalme 3

Muhtasari wa Video:

Mungu alimpa Mfalme Sulemani nafasi ya kuomba chochote alichotaka. Angeweza kuomba utajiri na heshima, lakini badala yake alimwomba Mungu ampe hekima ya kimungu ambayo ingemsaidia kufanya maamuzi ya busara katika kuongoza ufalme.

Muda mfupi baada ya Sulemani kuomba hekima, wanawake wawili walimjia wakihitaji msaada wake kutatua tatizo gumu. Kila mmoja alikuwa mama wa mtoto mchanga, lakini mmoja wa watoto hao alikuwa amefariki akiwa na umri wa siku tatu tu. Wanawake wote wawili walidai kwamba mtoto aliyekuwa hai alikuwa wao. Hili lilikuwa jambo gumu sana kwa Sulemani! Alipaswa kugundua ni yupi kati yao aliyekuwa mama halisi wa mtoto huyo.

Sulemani alipendekeza kwamba mtoto akatwe vipande viwili ili kila mama apate sehemu yake. Bila shaka, pendekezo hilo lilionekana la kushangaza na la kutisha kwa kila aliyelisikia! Lakini kwa sababu Sulemani alikuwa amepewa kipawa cha hekima kutoka kwa Mungu, alijua kwamba hatalazimika kutekeleza tishio hilo. Mwanamke aliyekuwa ameiba mtoto alikuwa mwenye ubinafsi na alikuwa tayari kuona tishio hilo likitekelezwa. Lakini mama halisi, kwa kuwa alitamani kumwokoa mwanawe, alikuwa tayari kumwachia mtoto huyo ili maisha yake yaokolewe.
Kwa hekima kubwa, Sulemani alijua kwamba mama halisi angefanya chochote ili kumlinda mtoto wake. Hekima ya Sulemani iliokoa maisha ya mtoto huyo, na akamrudisha kwa mama yake halisi.

 

Kuhusu Video:

Shela anamweleza mteja jinsi Mfalme Sulemani alivyokuwa na hekima na jinsi alivyotumia hekima hiyo kumtukuza Mungu. Anasimulia hadithi ya jinsi Mungu alivyompa Sulemani hekima wakati wanawake wawili walidai kwamba mtoto mmoja alikuwa wao.

Sulemani alikuwa mwana wa Mfalme Daudi. Daudi alikuwa mwaminifu na alizifuata sheria za Mungu. Ingawa hakufanya yaliyo sahihi kila wakati, alikuwa mnyenyekevu na aliomba msamaha alipokosea. Daudi alijulikana kama mfalme bora na mwaminifu zaidi katika historia ya Israeli.

Sulemani pia alitaka kuwa mwaminifu na kuzifuata sheria za Mungu. Alijifunza kutoka kwa Daudi kwamba kuwa mfalme na wakati huo huo kumfuata Mungu si jambo rahisi, hivyo alitambua kwamba alihitaji hekima kutoka kwa Mungu.

Mungu alimpa Sulemani hekima, lakini Sulemani alipaswa kuchagua kubaki mwaminifu kwa Mungu. Alipomwahidi Sulemani hekima, utajiri na heshima, Mungu alimwambia, "Na kama utakwenda katika njia zangu na kushika amri na maagizo yangu kama Daudi baba yako alivyofanya, nitakupa maisha marefu." (1 Wafalme 3:14).

Maswali ya Kutafakari:

1. Kwa nini Sulemani alimwomba Mungu ampe hekima?

2. Sulemani alitumiaje hekima yake kutambua mama halisi wa mtoto?

3. Unadhani mama halisi wa mtoto alihisije Sulemani alipendekeza mtoto akatwe vipande viwili?

4. Kama ungepewa nafasi ya kumwomba Mungu akupe kitu chochote, ungemwomba nini? Kwa nini?